Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:Kuhusiana na kuendelea ushirikiano wa Washington na Riyadh, msemaji wa Pentagon amesema kuwa, sisi tutaendelea na ahadi yetu ya kuihami na kuiunga mkono Saudi Arabia kwa nguvu zote. Saudia imekuwa ikishambuliwa na hakuna shaka katika hilo.
Matamshi hayo ya John Kirby yanaashiria mashambulio ya hivi karibuni ya ndege zisizo na rubani na makombora ya wanamuqawama wa Yemen dhidi ya ngome na taasisi za Saudi Arabia na madai ya Washington ya kuuunga mkono utawala wa Aal Saud mkabala wa mashambulio hayo.
Kwa hakika msimamo huu wa Washington unaweza kuonyesha wazi utendaji halisi wa serikali ya Joe Biden mkabala na Saudi Arabia. Baada ya kuingia madarakani Joe Biden kufuatia kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Rais wa Novemba mwaka jana (2020) nchini Marekani, yeye na baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali yake kama Antony Blinken waziri wake wa Mashauri ya Kigeni walionyesha misimamo ambayo iliashiria kwamba, Washington inafikiria upya uhusiano wake na serikali ya Riyadh. Kufuatia ishara hizo, fikra za waliowengi ulimwenguni zilikuwa zikitaraji kwamba, kutatokea mageuzi ya kimsingi katika uhusiano wa pande mbili hizo.
Hata hivyo hivi sasa imefahamika wazi kuwa, licha ya ahadi hizo, sera kuu na jumla za Marekani kuhusiana na Saudia ikiwa muitifaki mkuu wa Washington katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi, zinngali zinapita katika mkondo ule ule wa uungaji mkono wa pande zote na kuikingi kifua Saudia.
Aidha licha ya kuweko misimamo mikali hapo awali ya Biden na timu yake ya uongozi katika serikali yake kuhusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi mwana habari mtajika na mkosoaji wa Saudia, hivi sasa utashi na upendelezo wa kisiasa, kiuchumi na kistratejia umeifanya serikali ya Biden isimchukulie hatua Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia aliyetoa agizo la mauaji hayo.
Msimamo huu wa kindumakuwili wa Marekani unaonyesha wazi, utambulisho wa ria na kujionyesha wa Biden kuhusiana na suala la haki za binadamu. Katika mahojiano yake na vyombo vya habari, Biden amesema hawezi kumuita Bin Salman kuwa ni muuaji, kwani Saudia ni mshirika wa Marekani. Amesema, hivi sasa Saudia imo mbioni kutekeleza orodha ya mambo ambayo Marekani inataka Riyadh iyafanye.
Pierre Sprey, mchambuzi wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) anasema: Mimi nina uhakika kabisa kwamba, jambo la kwanza katika orodha hiyo ya Washington ni Saudia kutakiwa inunune silaha kutoka kwetu.
Licha ya kuwa serikali ya Biden imesitisha kwa muda kupeleka silaha huko Saudia kutokana na kuendelea vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen, lakini usimamishaji huo unahusiana tu na silaha za mashambulio. Ni kwa sababu hiyo na kwa kisingizio cha kuendelea mashambulio ya Wayamen dhidi ya Saudia, ndio maana serikali ya Biden imetangaza kuwa, itaendelea kuiimarisha kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu.
Hatua ya Saudia ya kuelezea wasiwasi ilionao wa mashambulio ya hivi karibuni ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Wayamen dhidi ya taasisi za mafuta inafuatulia kupatiwa misaada zaidi kutoka kwa Marekani.
Gazeti la Marekani la Wall Street Journal Alkhamisi iliyopita lilitoa ripoti inayoonyesha kuwa, serikali ya Washington imeunda jopokazi ambalo litaainisha njia ambazo kupitia kwazo itawezekana kusaidia suala la kuhami na kulinda miundomsingi ya Saudi Arabia mkabala na mashambulio ya wanamuqawama wa Yemen. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, machaguo yanayozungumziwa ni pamoja na kuiuzia nchi hiyo ya Kiarabu silaha hususan zana za kiulinzi kama rada za kunasa makombora, ushirikiano wenye wigo mpana wa taarifa za kiintelijensia, mafunzo ya ziada na mikakati ya ubadilishaji wanajeshi.
Kwa muktadha huo, licha ya agizo la Joe Biden la kuondolewa mifumo yake ya ngao ya makombora ya Patriot kutoka Saudi Arabia, lakini misaada ya kijeshi yenye wigo mpana kwa Saudia itaendelea.
Hii inaonyesha utambulisho wa kindumakuwili wa serikali ya Joe Biden mkabala na Saudia na kimsingi ni sisitizo kwa mara nyingine tena juu ya suala hili kwamba, kigezo kikuu cha Washington katika uhusiano wake na Riyadh ni maslahi, malengo ya kiuchumi na kistartejia.
Licha ya madai ya kuheshimu haki za binadamu yanayotolewa na serikali ya Joe Biden, lakini utashi wa kisiasa na kutanguliza mbele maslahi ya Marekani ya kifedha na kistratejia kupitia kuiuzia silaha Saudia ni mambo ambayo yanazuia kuchukuliwa hatua yoyote ile ya kutaka kuhafifisha uhusiano wa Washington na utawala vamizi wa Saudi Arabia.
342/